Saturday, March 24, 2012

Hawajui kutafuta

Ni mengi wameyaua, mitaji iliyokuwa,
Midasi wanshakua, si dhahabu tope huwa,
Wote tumejionea, mwataka kusimuliwa?
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

COSATA waliiua, kisa yao kali njaa,
STC haikukaa, marehemu inshakua,
RTC zikaliwa, hadi zote zikavia,
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

SUKITA ilitanua, hai tukaitarajia,
Wajanja walipoingia, ikaanza kuugua,
Siku walipozichomoa, hakuna kilichobakia,
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

Wanauza masalia, wajanja wanakwapua,
Uoza uliokuwa, matunda yake ni haya,
Na kila anayejua, heshima imepotea,
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

Ushirika wakaua, wengine kusingizia,
Maskini Tanzania, nyongo yatutumbukia,
Kila kinachozaliwa, kichanga bado huuawa,
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

SACCOS tulizinyanyua, wao wakazitegea,
Chini mwelekea kutia, ila kutokuendelea,
Unafiki wajitia, kila mtu anajua,
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

Utajiri tukiukwaa, wao wanatuhofia,
Tena hatutawasikia, yetu tutazingatia,
Na ndivyo inavyokua, katika hii dunia,
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

Vyama vinavyobabia, na dira zilizopotea,
Nchi kuishikilia, umaskini wavutia,
Wao wataung'ang'ania, nusura kujiokoa,
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

Sasa watu wanajua, ukweli ulivyokuwa,
Haya wanayakataa, vigumu kuendelea,
Nchi wataka kulea, sasa ipate kukua,
Hawajui kutafuta, wajua kula mitaji!

Wageni wawatumia, misingikusimamia,
Nami nashuhudia, kwalo wameshapotea,
Pabaya tutaishia, kama si kesho ngojea,
Hawajui kutafuta, uchumi wanauua!

No comments: