Saturday, March 24, 2012

Huharibu watokako

Ni hadimu walioko, nyuma wasoangalia,
Huathiri watokako, huku wakijivunia,
wasijue ni wanoko, mbele yatayotokea,
Huharibu watokako, kurudi pasiwe njia!

Njozi zao machafuko, amani hawajajua,
Na ruhusa kwao mwiko, h aki hawajatambua,
Uzazi kwao maziko, na bahati ni balaa,
Huharibu watokako, kurudi pasiwe njia!

Si watu wa maitiko, hawana la kuzingatia,
Ni watu wa matambiko, jana yao ni hakika,
Hawajui waendako, kurudi nyuma tabia,
Huharibu watokako, kurudi pasiwe njia!

Si watu wa mapumziko, zawakimbiza ruia,
Kazi ni mahangaiko, kwenye dhiki huishia,
Hatima yao ukoko, wali wanaukimbia,
Huharibu watokako, kurudi pasiwe njia!

Huharibu watokako, wakashindwa kurejea,
Na huko sasa waliko, mali ikawaishia,
Yaanze masikitiko, na lawama kununua,
Huharibu watokako, kurudi pasiwe njia!

No comments: