Tuesday, March 27, 2012

Twafa mara mbilimbili

Haiwezi kuwa hoja, ila kwa walio dhalili,
Katika kufunga mkaja, mitihani hukabili,
Akili bure hufuja, panapohitaji musuli,
Twafa mara mbilimbili, nini kufa mara moja?

Watu hufa kwa kungoja, pamwe na ya leo hali,
Majuja na Maajija, nao hawatayahimili,
Vilemba nayo makoja, ya uongo si halali,
Twafa mara mbilimbili, nini kufa mara moja?

Watu hufa kwa kufuja, na wengine ubahili,
Mbinafsi wetu mja, na yake si ya wawili,
Anaikosa daraja, kwa kuwa ndumilakuwili,
Twafa mara mbilimbili, nini kufa mara moja?

Watu hufa kwa useja, na wengine wanawali,
Walafi wana mirija, tena miwili miwili,
Hufanza lisilo haja, wakaacha bilkuli,
Twafa mara mbilimbili, nini kufa mara moja?

Watu hufa kwa magonjwa, na wengine mankuli,
Wapo wapendao ganja, lakini hutupa wali,
Wanywao chupa moja, wengine kumi na mbili,
Twafa mara mbilimbili, nini kufa mara moja?

Wapo wasio faraja, misaada ni aghali,
Na wanaopiga mbinja, kwenye bohari ya mali,
Bahari yao kuvuja, huwa ni kitu muhali,
Twafa mara mbilimbili, nini kufa mara moja?

Haweshi wanaokuja, na kuondoka shughuli,
Kitamu anayeonja, huiogopa shubili,
Na kinyume cha mjanja, huwa mtu anzali,
Twafa mara mbilimbili, nini kufa mara moja?

No comments: