Tuesday, March 27, 2012

Wakubwa si malaika

ZAMANI kuna hadaa, sinema iliyokuwa,
Wakubwa tulidhania, watu wema wanakua,
Watukufu tukajua, hata kuwasujudia,
Wakubwa si malaika, uongo usikubali!

Hasa wanaotumiwa, watu kuwanyanyapaa,
Uroho waliojaa, ukubwa kujilimbikia,
Na uchu kuupakua, mlo wote kujilia,
Wakubwa si malaika, uongo usikubali!

Kuna wakubwa balaa, wizi wamejisomea,
Huwaibia raia, fukara wazidi kuwa,
Wakadhani mashujaa, kumbe ni tupu fedheha,
Wakubwa si malaika, uongo usikubali!

Kura zikihesabiwa, mabingwa wa kuhadaa,
Yao kwao hujipangia, hadi washindi wakawa,
Mate anawatemea, Mola akiangalia,
Wakubwa si malaika, uongo usikubali!

Waongo pia wajaa, Afrika nawambia,
Na dhambi huwarudia, kwa wengine kusingizia,
Mola hawajamjua, hatoweza kusinzia,
Wakubwa si malaika, uongo usikubali!

Katiba huwaibia, wamiliki walokuwa,
Ujivuni kujitia, na ujibari kuvaa,
Shahidi ashuhudia, kiyama chawangojea,
Wakubwa si malaika, uongo usikubali!

Wapo wanaong'aa, mchana unapokuwa,
Usiku ukiingia, mashetani wanakuwa,
Free Masons mwajua, jina wameshagaiwa,
Wakubwa si malaika, wengine ngono tabia!

Ziara zinatumiwa, uchafu kujifanyia,
Huzungukwa na zinaa, kila njia ya hatua,
Malaika humkimbia, baharini kwenda kaa,
Wakubwa si malaika, wengine mashoga pia!

Hawana la kuhofia, kaumu Lutu ikiwa,
Wachache waliokuwa, yao hujizawadia,
Ila nchi hulaaniwa, ikaja kuadhibiwa,
Wakubwa si malaika, wengine ni wasagaji!

Kalakhi twakuangukia, inusuru Tanzania,
Cha kufanya wakijua, hatuna tunalojua,
Salama tunaililia, wakiwa tuliokuwa,
Wakubwa si malaika, wengine kumbe waovu!

No comments: