Tuesday, March 6, 2012

Hunijui, sikujui

Sababu mimi sijui, kuipata cheichei,
Sikujui, hunijui, iwe ndiyo baibai,
Uliache baibui, sitaki ona wajihi,
Hunijui, sikujui, tuachane vivi hivi!

Sitaki ona wajihi, japo hijabu huvai,
Naomba unistahi, nami nitakustahi,
Katika wangu uhai, sipendi yenye nishai,
Hunijui, sikujui, tuachane vivi hivi!

Hunidai, sikudai, hatuazo tanabahi,
Mtu humu haingii, kama moyo humjui,
Nje utajistahi, na kuondoka uwahi,
Hunijui, sikujui, tuachane vivi hivi!

Kwako mimi sina rai, za kwangu hazikufai,
Ni mbali mwanajamii, siutaki usanii,
Ungejua yangu bei, dukani usingewahi,
Hunijui, sikujui, tuachane vivi hivi!

Ninatoka kwenye nai, ninakwenda matlai,
Ninaifuata chai, pia na wali wa tui,
Na ugenini sikai, kama si namna hii,
Hunijui, sikujui, tuachane vivi hivi!

Hushtuka majeruhi, akikuta makuruhi,
Na shiriki haifai, kwani mkweli hakai,
Kama mtu humjui, zima kwanza yako nai,
Hunijui, sikujui, tuachane vivi hivi!

No comments: