Tuesday, March 6, 2012

Ikifika kumi sepa

KUMI sepa ikifika, au utanilaumu,
Toka mwana ukitoka, nami nishike taimu,
Mlango ukifugika, kurudi nyuma haramu,
Ikifika kumi sepa, au utanilaumu!

Kuishi hapa mashaka, bure utanilaumu,
Waezua naezeka, ni nani akae humu,
Hebu nenda lalko shika, naona hujifahamu,
Ikifika kumi sepa, au utanilaumu!

Kila mkosa shaka, haishi kujituhumu,
Si wa kuongozeka, yu mbali mustakimu,
Dhambi zimeshamteka, wala si wa kujifahamu,
Ikifika kumi sepa, au utanilaumu!

Yake yamemalizika, dunia haina hamu,
Yangojea kumzika, aende kwao kuzimu,
Amekwishakengeuka, dua kwake si muhimu,
Ikifika kumi sepa, au utanilaumu!

Latifu nimetamka, nawe ndiye tu Alimu,
Yangu yanatabirika, na mengine sifahamu,
Niepushe na gharika, katika hii kaumu,
Ikifika kumi sepa, au utanilaumu!

Kulia nalazimika, na kuishi sina hamu,
Naona nimeshachoka, na wala sio muhimu,
Riziki yamalizika, imebaki milizamu,
Ikifika kumi sepa, au utanilaumu!

No comments: