Sunday, March 4, 2012

W A K A T I

Tumia huu wakati, papa hapa katikati,
Ufanze yako ya dhati, kwa makubwa na katiti,
Muda usiusaliti, ukajuta kalimati,
Ukipita huukuti, ndio siri ya wakati!

Wakati hauna hati, umiliki kwa shaarti,
Wakati ni mahluti, mchanganyiko wenye nyeti,
Hautaki tashtiti, wataka umadhubuti,
Ukipita huukuti, ndio siri ya wakati!

Haukubali mageti, kupita kwa udhiiti,
Hata katika baiti, hutoka bila shuruti,
Tashili yake ya nyati, akitoka humkuti,
Ukipita huukuti, ndio siri ya wakati!

Funga nati na boriti, katikati hausiti,
Vuta kwako huuvuti, hata uwe na umati,
Wepesi wake wa jeti, kwenda mbio ni spoti,
Ukipita huukuti, ndio siri ya wakati!

Maelezo huyapati, wala majambo huteti,
Upweke umetaiti, ya kwake hauyasuti,
Halifunguki kabati, lake toka Maskati,
Ukipita huukuti, ndio siri ya wakati!

Tamu kama biskuti, au pipi za markiti,
Ikiwa umetafiti, na kwa raha umeketi,
Unapata malimati, na uhondo wa tikiti,
Ukipita huukuti, ndio siri ya wakati!

Taabu zikisaliti, kama shubiri hutweti,
Uchungu hauupati, maisha huwa mauti,
Na upendo na mapeti, kwako tena hawatakati,
Ukipita huukuti, ndio siri ya wakati!

No comments: