WANAZO kauli mbiu, zakupasha hujajua,
Wakubali walo juu, vigumu kusaidia,
Kama wataka nafuu, budi kuipigania,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hakuna cha serikali
Kama ipo siamini
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Ardhi kukunyanyua, vitani unatakiwa,
Kwa pamoja kutambua, haki yenu mtapewa,
Mkigawanyika baa, hamuwezi ambulia,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hakuna wanasiasa
Kama ipo siamini
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Kilimo kije chanua, kuuza nje yafaa,
Walanguzi kuondoa, wenyewe kujiuzia,
Mkaipata jalia, msije kupungukiwa,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hakunacho cha wabunge
Kama ipo siamini
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Kijiji kuendelea, vinara bora chagua,
Waovu mkiachia, mtazidi didimia,
Chagua kuendelea, sio kuchanganyikiwa,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hamna chama cha siasa
Kama ipo siamini
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Mitaa misafi kuwa, babaisha kuondoa,
Tenda wapate kupewa, kazi wanaoijua,
Na zana navyo vifaa, vikawa si vya sanaa,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hakuna cha uwaziri
Hawezi ishi milele
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Kipato kujiongezea, chakarika bila haya,
Hakuna wa kukutoa, mwenyewe utajitoa,
Panga zote zako gia,
Ukianzia waishia,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hakuna chake tajiri
Kama ipo siamini
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Umoja ukichanua, mtayapata maua,
Mmoja mmoja mkiwa, rahisi kuzainiwa,
Maarifa kujifia, na juhudi kufukiwa,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hakuna cha mfadhili
Kama ipo siamini
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Amani haijazaliwa, twalea historia,
Ili kuichangamkia, uchumi kushikilia,
Hayo yasipotokea, isubiri Tanzania,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hakuna chake msomi
Kama ipo siamini
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Isubiri Tanzania, amani ipate jua,
Ya thamani asilia, isiyochakachuliwa,
Na kisha kuyaridhia, leo ninayowaambia,
Ukombozi kazi yako, budi kuifanya wewe:
Kiuchumi, kijamii
Hakuna chake mzungu
Kama ipo siamini
Zitakuja, zitatoka
Nawe upo papo hapo
Wapiga maktaimu !
Machi 4, 2012
Dar es Salaam. Tanzania
Sunday, March 4, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment