Monday, March 26, 2012

Vyoo vya Chuo Kikuu

Mtihani nautoa, wote ni watahiniwa,
Utafiti kuandaa, Chuo Kikuu ukawa,
Tupate sote kujua, kama kiwango twafaa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Kufunga wameamua, afya wanaohofia,
Vyoo sasa ni balaa, harufu yaweza kuua,
Vinyesi vyatapakaa, ni maua yamekuwa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Wengine wameamua, ratiba kujiwekea,
Safari kujifungia, nyumbani kwenda jifaa,
Mara tatu watimua, vyoo kwao kutumia,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Mbali wanaotokea, msiba kwao imekuwa,
Hawanalo la kugwaya, vijijini wamezoea,
Kuchimba dawa tabia, si ajabu Tanzania!
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Holi faivu twatua, vyooni tunaingia,
Mlango ukifungua, na ndani ukaingia,
Ukiweza jisaidia, maksi wazawadia,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Chooni atakayekaa, digrii atapewa,
Kafaulu kwa kinyaa, kiumbe kuvumilia,
Kutoka kikikataa, huna cha kuambulia,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Wasomi tungedhania, viongozi walokuwa,
Na nje wameshakaa, vyoo wamejionea,
Haya wasingevumilia, kwao ingekuwa balaa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Migomo waichukia, si vyoo vyenye kinyaa,
Ukubwa wafurahia, nyuma ni harufu mbaya,
Hekalu wajijengea, wao na zao jamaa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Wahindwa kuangalia, ya walio wengi afya,
CIA wamekuwa, migomo kuizuia,
Na chama wakitumia, kinyesi wakipakaa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Tivii yao najua, chooni haijaingia,
Laiti ingelijua, hali bora ingekuwa,
Labda waambiwa, hawawezi kuingia,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Au juu waliokuwa, uganga wanatumia,
Kila anayeingia, usafi ajionea,
Ibilisi kubwa dawa, hasa wenye roho mbaya,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Au wanaogopewa, mabaya kutoambiwa,
Na mazuri wasifiwa, na wapambe walokua,
VC lini kuingia, chooo chao raia?
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Au wameteuliwa, shemeji waliokuwa,
Na ndugu zao kujaa, rafiki nao jamaa,
Na wanachokiangalia, safari zao Ulaya?
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Zuri ninalingojea, si watu kuhujumiwa,
Sadaka nimeitoa, chuo kiweze jaliwa,
Daraja juu kupaa, cha kimataifa kuwa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Usafi ukishaingia, chuo kikuu kikawa,
Mpaka msingi pia, sekondari kufikia,
Na taasisi mamia, hali bora ikishakuwa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Na taasisi mamia, kimataifa zikawa,
Ruhusa nitaitoa, uranium kuchimbua,
Usalama nitajua, kweli sasa wazingatiwa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Kabla hamjachimbua, madini mnayotuibia,
Chuo kikuu kutua, vyoo kukarabatiwa,
Kwa hilo tutaelewa, mema mwaanza tutakia,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Wiki ninawaachia, kwa vyoo kutengemaa,
Au picha nachukua, kutangazia dunia,
Hadhi mkaondolwa, na madoa mkatiwa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

Vya msingi vyatakiwa, wengi vinawaofaa,
Ubinafsi kinyaa, kama kinyesi na njia,
Kiumbe hawezi kua, unafsi alojaa,
Kipimo cha Uranium, vyoo vya Chuo Kikuu:
Tukachimbue au la!

No comments: