Monday, March 26, 2012

Mzungu akikujua

Hiy9 ni yake tabia, toka alipozaliwa,
Watumwa huwatumia, ya kwake wakamfaa,
Kaigeuza dunia, tambaa kujifutia,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Nasaba walozaliwa, watumwa waliokuwa,
Kasumba inakolea, vigumu kuwaondoa,
Bado wanyenyekea, mweupe kumtegemea,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Huwapuuza wazawa, na tena wakawagawa,
Nchi wakaachia, wazungu wasiojua,
Na tenda wakazitoa, kwa zuzu nao majuha,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Wanachofuatilia, pasenti wanayopewa,
Mengine kwao udhia, nchi hii yawapwaya,
Benki wakizichukua, Ulaya wanahamia,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Wana huwagharamia, elimu ya kujijua,
Waende kutojijua, na kurudi wasiojua,
Na urithi huachiwa, na wafalme walokuwa,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Sinema za Kinigeria, hili zinalitambua,
Ona shere kuchezewa, mweusi anavyotanua,
HJku njaa wajifia, ndugu zao walokuwa,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Ni Urussi iliyokuwa, na sasa yamerudia,
Wafalme watumia, raia wararuliwa,
Ufaransa nako pia, hadi mapinduzi kuwa,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Afrika yalemaa, kwa mbeleko ya Ulaya,
Na kila mwenye kujua, hili atalikataa,
Vijana ninawaambia, msije mkachelewa,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Sanaa watuulia, sasa nyani tumekua,
Twaiga yasiyokuwa, na tena yasiyofaa,
Weusi hautakuwa, weupe ninawaambia:
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Lugha wanatuulia, na elimu kudidimia,
Watoto twawaonea, Kiingereza kutumia,
Kusoma sio kujua, lugha ya mama si bia,
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Lugha ni kujisomea, nyingi tu ukazijua,
Maabara zatumiwa, sayansi na teknolojia,
Miezi haba yafaa, hata mbili ukajua:
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Mashariki twatakiwa, tuanze kueleka,
Kichina tukakijua, nacho pia Kimalaysia,
Kadhalika na India, Gujarati kuongea:
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!


Ila kwa kufundishia, ni ya mama kutumia,
Rohoni inaingia, na vitu vingi kujua,
Moyoni hukubaliwa, kama mbegu vikakua:
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

Ninamuomba Jalia, nusura kutupatia,
Kutoa wanaosinzia, tupate wanaozua,
Bure tunayoyaua, na wenyewe kujifia:
Mzungu akikujua, wapenda utegemezi:
Haachi kukutumia
Mtumwa kwake ukawa
Na kisha hukudharau!

No comments: