Monday, March 19, 2012

Asante wabunge wetu

(Ustawi wa zahama)

Wana zao jenereta, TANESCO wakizima,
Kwa kelele zatokota, rabsha mtaa mzima,
Klabu, pabu waita, nao waliona jema,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Starehe wameleta, yafaa watu wazima,
Ila sasa zinapeta, hata kwa wasio wazima,
Fujo na mengi matata, imekuwa ni zahama,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Changudoa wamevuta, Ohio wameihama,
Uchi watu huwakuta, njiani wamesimama,
Imegoma kalkuleta, idadi ningelituma,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Walevi zawaburuta, sinema kuzitazama,
Alama zilizofutwa, kila mtu atazama,
Na wengine wakidata, mpira kuja tazama,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Kufeli sasa sakata, watoto mtaa mzima,
Usingizi kutopata, hivi vipi watasoma?
Balaa mmeileta, na nyinginezo tuhuma,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Na haya yote matata, wanakitumia chama.
Nuksi kwa kuzileta, eti ndio kimewatuma,
Maendeleo kupata, ambayo kwetu nakama,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Kwenye sala tunatota, miziki inavyorindima,
Uradi huwezi vuta, kelele hukusakama,
Na dua ukiiteta, ni makosa chungu nzima,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Msikitini twateta, kinaingia kiyama,
Na wao wanatusuta, akili zimeshatuhama,
Wakati eti ukuta, hizi ndio zao zama,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Vijana watuchakata, ruksa kuzisukuma,
Huko waenda kufata, ya mpira na zahama,
Changudoa wawanata, watoto sio wazima,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Wazee wamefyata, usingizi waparama,
TANESCO wakikata, umeme wa jimbo zima,
Wengine wajikunyata, si baridi ila njama,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Usingizi kuupata,kazi kubwa kutwa nzima,
Vyovyote wautafuta, maisha sasa mrama,
Wengine waanza teta, kwenda hamia Butiama,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Viongozi wanasita, posho inawatazama,
Leseni wakizifuta, njaa itawasakama,
Sasa kelele za vita, zinasikika kwa nyuma,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Chao waliokwishachota, njiani wameshakwama,
Hawawezi kusogea, na jua lazidi kuzama,
Kila atakaye pita, huwa arudishwa nyuma,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

Mutumaina naita, jahazi lisije zama,
Maji tuanze kuchota, nje tuakayasukuma,
Kwa salama tukapita, njia isiyo salama,
Asante wabunge wetu, Segerea na Ilala:
Muziki hadi manane, kulala sio ruksa!
Klabu, pabu kuleta!

No comments: