Mimi kiumbe dhalili, tena dhoofu kwa hali,
Ya kwangu yanikabili, ya wengine sihimili,
Kalima yangu amali, kuchuma natajamali,
Niafu wangu Jalali, kiumbe natarajali!
Sikujaliwa akili, ilo kwa yako adili,
Nilohodhi taamuli, ni yako wewe Jalali,
Kwangu mimi mhimili, bila yake sina hali,
Niafu wangu Jalali, kiumbe natarajali!
Sinao wingi wa mali, Allahadulillahi,
Ulichonipa wakili, kinanitosha rijali,
Kizazi nakisaili, kuitumia akili,
Niafu wangu Jalali, kiumbe natarajali!
Vipo zaidi ya mali, wallahi umenijali,
Navyo kwangu ni amali, kisha mema na ukweli,
Na hivi rasilimali, utajiri nakabili,
Niafu wangu Jalali, kiumbe natarajali!
Usinifanye bahili, kwa fakiri na ahali,
Mimi kwao ni kandili, japo nishati aghaali,
Kitunze kiwiliwili, ya kwao kuyadahili,
Niafu wangu Jalali, kiumbe natarajali!
Nizawadie fasili, na utunzaji asili,
Niweze kutajamali, kwa ruksa Mutawakali,
Nipate si kalili, kaumu isijefeli,
Niafu wangu Jalali, kiumbe natarajali!
Ingawa dhoofu hali, unipe yako kabuli,
Kutenda yenye akili, na nyinginezo amali,
Waliodhofu hali, kunizidi kuhimili,
Niafu wangu Jalali, kiumbe natarajali!
Nmba yangu isajili, nipate yako kauli,
Niendapo nistahili, ya thamani na aghali,
Kwa kuwa leo dhalili, na dhoofu bin hali,
Niafu wangu Jalali, kiumbe natarajali!
Saturday, March 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment