HIVI sasa yatokea, vijijini nakokaa,
Mizizi wanaing'oa, matawi washikilia,
Hili ninalihofia, mti kuja kujifia,
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Ila wao wanambia, hii si ya jana dunia,
Yabadilika hatua, usiku mchana ukawa,
Hulka hali ya hewa, kugeuka majaliwa,
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Kila nikiangalia, nashindwa kuwaelewa,
Kila wapiga harua, nyuma huwa warejea,
Na juu waliokuwa, chini sasa washuukia,
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Majani ni kahawia, si kijani yanakuwa,
Yakauka na kuvia, ugoro kuelekea,
Na haya nayajua, mwisho yatakoishia,
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Jalala layangojea, maombi yeshakubaliwa,
Yataishi kwenye jaa, hadi yakawa mbolea,
Na atakayeitumia, bado sijamuelewa,
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Mizizi itaishia, kunyauka na kunywea,
Kuota tena najua, rahisi haitokuwa,
Labda ikiwa mnyaa, kufaurongo yajua,
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Mashinda yataishia, katikati kukatiwa,
Na kuni kuchukuliwa, nyumbani kwenda tumiwa,
Au kuchomwa mkaa, wenye majiko ku'ziwa
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Ingekuwa mtidawa, unga ungesagiwa,
Kwenye chupa wakatia, au mifuko kujaa,
Ngethwa kwenda tembea, werevu ikawafaa,
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Hesabu nahesabia, jumla sijaijua,
Na litakalotokea, lazima kuwaambia,
Hakiwi kisichokuwa, mizizi isipokuwa,
Matawi mwashikilia, mizizi mmeshaing'oa ?
Sunday, March 4, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment