Sunday, March 11, 2012

Kiyama timu za njaa

Kama nilivyowaambia, timu njaa hujifia,
Klabu zinazokuwa, michango zategemea,
Na vyeo hupiganiwa, watu kujiganga njaa,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Msiba wa kujitakia, watu bure wanalia,
Haya mlikwishaambiwa, na wale wanaojua,
Kiburi mkajitia, karimu kuwagomea,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Mengi angeichukua, Yanga mbali ingekuwa,
Azam juzi waingia, leo wawaporomoa?
Kwenye njaa mwaishia, na bado watawabomoa,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Mabingwa watarajiwa, kwa muda watabakia,
Mamluki walokuwa, siasa wakiutmia,
Ila ninawaambia, ndio kwanza waishia,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Klabu bingwa Tanzania, kampuni itakuwa,
Siasa inayokataa, na wengi kufadhiliwa,
Ngoma mmoja kutua, iwe inayokimbiliwa,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Bakhressa kaingia, wengine watafuatia,
Kuwekeza kuwa nia, na pato kujipatia,
Kuuza na kununua, wachezaji walokuwa,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Mameneja wenye njaa, mbali watatupiliwa,
Magwiji watabakia, kazi wanaoyoijua,
Kurudi nyuma najuu, rahisi haitakuwa,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Amkeni nawaambia, kadari kuiondoa,
Si punde mtafukiwa, msijue kinachotokea,
Ibakie historia, klabu ilipozaliwa,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Pangeni na kupangua, mitaji inatakiwa,
Viwanja kuvikamia, vya kwenu kujijengea,
Na shule kuzifungua, michezo kuendelea,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

Na timu nyingi zikawa, ndanindani zachezea,
Kwa umri kuzigawa, taratibu zikakua,
Na siku ikifikia, maajabu hutokea,
Kiyama timu za njaa, kimekwishakuwadia!

No comments: