Saturday, March 10, 2012

Mzoea kudowea

Yumkini nakwambia, kula chake hatoweza,
Mzoea kudowea, hilo linamtatiza,
Pengine utamdhania, keshakuwa ni ajuza,
Mzowea kudowea, kula chake hatoweza!

Hili sijalielewa, naona ni miujiza,
Vipi anapotowelea, asivyovitengeneza,
Lakini ikishakua,ni vyake sana vyamtatiza?
Mzowea kudowea, kula chake hatoweza!

Huwa kiguu na njia, vya watu kuviagiza,
Kope akazinyanyua, hadi kujitia giza,
Na macho kuyabania, na vingie kukonyeza,
Mzowea kudowea, kula chake hatoweza!

Chake ukimpakulia, kooni kinamkwaza,
Hushindwa kukitumia, njaa yake kutuliza,
Akawa aangalia, kama mwenye sumu pweza,
Mzowea kudowea, kula chake hatoweza!

Chakula hukiachia, hadi kuja kikaoza,
Harufu inapojaa, ndipo hujamgutuza,
Chungu akakinyanyua, nje kwenda patiliza,
Mzowea kudowea, kula chake hatoweza!

Ninashindwa kutambua, kushindwa kukichakaza,
Alichojitengenezea, hadi kiwe chapendeza,
Akawa nayo kinaya, kula iwe hatoweza,
Mzowea kudowea, kula chake hatoweza!

Mengi ninafikiria, labda kakiunguza,
Au kachanganyikiwa, chumvi nyingi kaongeza,
Au ugali wabwia, maji mengi amejaza,
Mzowea kudowea, kula chake hatoweza!

Au wali umejaa, mawe yanayotatiza,
Sijapata kuijua, sababu kutosheleza,
Ni maneno nasikia, nami yote nayapuuza,
Mzowea kudowea, kula chake hatoweza!

No comments: