Tuesday, March 27, 2012

Umfaaye hakufai

FAA unaowafaa, usingoje shukrani,
Hilo halitatotkea, sembuse wakuthamini?
Watu wapenda pokea, kutoa kwao mtihani,
Umfaaye hakufai, kwenye dhiki hukimbia !

Unapowasaidia, tia uko hasarani,
Kwa kipimo kutumia, chake hapa duniani,
Ila kwako hii njia, kuelekea maskani,
Umfaaye hakufai, kwenye dhiki hukimbia !

Tenda kama hujajua, tena halina thamani,
Na mtu kutoangalia, alivyokuwa usoni,
Shukrani akitoa, mwambie ampe Manani,
Umfaaye hakufai, kwenye dhiki hukimbia !

Watu ni kuwavumilia, ili usiwe shakani,
Wakwambiacho sikia, kufanya kitu imani,
Uwape nacho ukiwa, sio chako cha rehani,
Umfaaye hakufai, kwenye dhiki hukimbia !

Usije ukawatia, katika hiyo mizani,
Wa kweli waliokuwa, na waongo nukstani,
Mola ungemwachia, huwa ni kubwa hisani,
Umfaaye hakufai, kwenye dhiki hukimbia !

Usinune kujikwaa, pasiwe mwenye imani,
Juu akakunyanyua, akakuweka kitini,
Shukuru unachopewa, mengineyo ni ihsani,
Umfaaye hakufai, kwenye dhiki hukimbia !

Mbele ukiangalia, usije fika mwakani,
Kwanza toa inshallah, na hedaya ithamini,
Kinachowahi hutua, kabla kufika chini,
Umfaaye hakufai, kwenye dhiki hukimbia !

Moyo wako achilia, mshukuru na Bathini,
Hatua uliyofikia, hakika sio thakini,
Zaidi unachopewa, ungemuachia Manani,
Umfaaye hakufai, kwenye dhiki hukimbia !

No comments: