Monday, March 26, 2012

Nchi eti mwaongoza?

Mwajivuna kuongoza, swali ninawauliza,
Kitu gani mwaongoza, kila kitu twaagfza?
Hdi sindano ni viza, hatuwezi tengeneza?
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa unda sindano?

Nchi eti mwaongoza?

Trekta kutengeneza, hivi ni miujiza,
Wazungu tukiagiza, kazi zinazowaiza,
Hapa kwettu kuwatunza, kazi hii hawataweza?
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa unda trekta?

Nchi eti mwaongoza?

Plau tunaagiza, powertiller mwaeleza,
Kitu msichoeleza, kwanini kutotengeneza,
Usanii mwaagiza, rahisi vitu kuoza?
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa unda plau?

Nchi eti mwaongoza?

Mabasi yatutatiza, nini tunachokiweza,
Mbona China wameweza, na India watengeneza?
Wahandisi twawaponza, hawawezeshwi wakaweza?
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa unda mabasi?

Nchi eti mwaongoza?

Swaziland naeleza, sio inayojiweza,
Leo wanatengeneza, friji zenye kupoza,
Nishati jua hutunza, umeme imepatiliza,
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa unda friji?

Nchi eti mwaongoza?

Majiko tunaaagiza, badala ya kuengeneza,
Na kupika twawajuza, kila siku tunafanza,
Biashara yatokeza, bei ikiwa yasuuza,
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa unda majiko?

Nchi eti mwaongoza?

Umma tukiwafunza, umeme watatengeneza,
Wazawa trunawabeza, yankii twaagiza,
Wenyewe twajimaliza, twazidi kujilemaza,
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa fuma umeme?

Nchi eti mwaongoza?

Roho tunaziuza, baharini Tanzania,
Tumeshindwa kuongoza, meli kutengeneza,
Wahandisi twalemaza, bilioni twapoteza,
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa kuunda meli ?

Nchi eti mwaongoza?

Ndege zitatumaliza, mitumba tulizoagiza,
Wenyewe twajichuuza, wajanja tunajifanza,
Yatakujatupatiliza, angalizo nawatunza,
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa kuunda ndege ?

Nchi eti mwaongoza?

Wachina tusipowaiza, reli tutatengeneza,
Na tena tukaifanza, ya kisasa muujiza,
Umeme ikasambaza, na haraka kufikiza,
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa kujenga reli ?

Nchi eti mwaongoza?

Barabara zatitia, wajenzi wa kuteua,
Zenyewe hujibomoa, wakubwa wakitembelea,
Nao wameshuhudia, ukweli wanaujua,
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa kujenga njia ?

Nchi eti mwaongoza?

Viwanja vya burudani, na pia vya kucheza,
Bado tumasikini, hali hili twaliweza,
Huu kama si uhuni, nini mtanieleza?
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa jenga viwanja ?

Nchi eti mwaongoza?

Bandari zina kinyaa, na sura zake ni mbaya,
Hata nilipowaambia, kidogo tu mmeangalia,
Hali yaweza ikawa, na sura za kuvutia,
Nchi eti mwaongoza, mwashindwa jenga bandari?

Nchi eti mwaongoza?

Kujenga pia twaweza, nia yetu bado mbaya,
Umasikini twaukuza, sera zetu kwendelea,
Hali ukweli najuza, hili si la kuchezea,
Nchi eti mwaongoza,watu wanakosa nyumba?

Nchi eti mwaongoza?

Njia zipo nyingi sasa, nishati kujivunia,
Ila naona twasusa, akili kuzitumia,
Wananchi twawatesa, hali sisi twatanua,
Nchi eti mwaongoza, wanaikosa nishati?

Nchi eti mwaongoza?

Maji tutakuja agiza, kama tusipoangalia,
Ajizi tunaifanza, watu kutaka jifaa,
Wajanja twawaachia, na sasa wanatunyoa,
Nchi eti mwaongoza, watu wanakosa maji ?

Nchi eti mwaongoza?

Nyingine ni za kupuuza, akili zisizokuwa,
Akili zenye kuzoza, ya yale yasiyokuwa,
Nani upate mjuza, ajira zimepotea?
Nchi eti mwaongoza, vijana hawana kazi?

Asalam aleykum

No comments: