Tuesday, March 27, 2012

Jenereta

MRADI uliobakia, kuuza majeneereata,
Rahisi kuyanunua, na kuongeza ukata,
Watu wakiwa na njaa, lazima watatufuata:
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

Hatuogopwi kusutwa, hadaa kwetu tabia,
Pindi tunapotafuta, ncha butu kwetu huwa,
Usiku twameremeta, hata nyota kuzidia,
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

Unapozidi ukata, hata ngebe huibua,
Chuma ulete twateta, budi kuiganga njaa,
Ushindi tusipopata, riziki itapotea,
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

Hununua jenereta, wenyewe kujiuzia,
Haiwi kwetu sakata, mipango twajisukia,
Huwaondoa vimeta, pindi wakiingia,
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

Sisi nani kujaleta, ustawi Tanzania,
Wakati kwetu ukuta, nasi twajitafutia,
Kukosa sio kupata, hatutaki nyeng'enyea,
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

Hebu lete kalkuleta, hesabu kukokotoa,
Hadi mwaka ukipita, bilionea nimekua,
Huwezi nyuma nivuta, ufukura nakimbia,
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

Nchi nitaikokota, ipate kuendelea?
Nache wengine kupata, mimi nife kwa njaa?
Utu huo nakeketa, siwezi ukubalia,
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

Zachanua jenereta, hapa kwetu Tanzania,
Kelele zinazoleta, na hewa kuichafua,
Mradi sisi twapata, haya tunavumilia,
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

Jenereta, jenereta, huree Watanzania,
Ukikosa utaokota, nafuu bei ikiwa,
Usiyahofu mafuta, karibu tutajichimbia,
Mradi wa jenereta, unakua Tanzania:
Hao waliouleta,
Wanaongeza ukata,
Laana zetu wapata,
Yajewachoma mafuta,
Ambayo wayatumia!

No comments: