Monday, March 26, 2012

Achia rasilimali

Siasa mnatumia, makapi mtabakiwa,
Sanaa nimesomea, na ukweli naujua,
Vingine haitakuwa, ila kujiharibia,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Bora ukiwachukia, kwa akili kutumia,
Waoga ukachukua, upate kuwatumia,
Naapa utafulia, na mbali hautafikia,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Taylor hutomjua, na Fayol ni ruia,
Demming nikikwambia, nokiauti nakutoa,
Sembuse gwiji radhia, Drucker aliyekuwa?
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Rasilimali ni njia, kila pembe kuingia,
Siasa, uchumi pia, kingine hakitafaa,
Na hasa kama ikiwa,ni watu wa kuamua,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Hawa waonyesha njia, taasisi ikakua,
Si kila mtu afaa, nafasi kushikilia,
Wapo waliozaliwa, maalum walokuwa,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Wengine wamejaliwa, wa kula na kutumia,
Hawawezi angalia, chochote kipate kua,
Ila wao kujilia, hilo kweli wanajua,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Wakubwa nawashangaa, kamba walioshilia,
Sasa wanaiachia, farasi ajiendea,
Na kitakachotokea, sote tunatarajia,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Fedha ukiwamwagia, shimoni zinaingia,
Chini kwenda didimia, ndio itakuwa tabia,
Hakuna wa kuzuia, 'freefall' inakuwa,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Hakuna wa kuzuia, 'freefall' inakuwa,
Wang'eng;e nawaachia, bungeni waliojaa,
Hili kuwatasiria, raia msiyoyajua,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

Razaki namtambua, kwake hili nimejua,
Wala sitaki umbeya, kwingine kusingizia,
Nami namkubalia, mwanga wake natumia,
Achia rasilimali, watu bora ilokuwa:
Na taasisi huvia!

No comments: