Saturday, March 31, 2012

Kila muabudu pesa

MWISHO huja kuikosa, kila muabudu pesa,
Kila kitu humsusa, akabaki hana hisa,
Muflisi kutonesa, liporomoke darasa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Huzitamani anasa, aanze naye kutesa,
Akaziacha fursa, vyenye pato kuvinusa,
Akahama kudodosa, ahamie kutomasa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Huwa ni kisa na mkasa, tena visivyo msasa,
Abakie kipukusa, ndizi isiyo hasusa,
Mwilini akipapasa, akute hanayo hisa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Hisia haiwi hisa, wala halipi posa,
Mchumba utamkosa, ambebe bwana Issa,
Na mwishowe ukasusa, ndoa uache kabisa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Kosa halijawa kosa, hadi kurudia kosa,
Baraka ikikigusa, nusura huwa mkasa,
Ya jana yakawa sasa, mtu uzidi kutesa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Pamoja kujipapasa, shilingi nimeikosa,
Koti nimeshalinusa, bado siioni pesa,
Na chini nimetikisa, naona yote mkasa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Watu huja kuwatesa, kila muabudu pesa,
Akakopa na kususa, madeni yakawa h isa,
Na kokote mkunusa, harufu mtaikosa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Mtaenda kwenye misa, na masjidi kugusa,
Dua mtie vitasa, bado huwa ni makosa,
Nyusi akishapepesa, yote huwa yake hisa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Ukitaka kumgusa, hupasuka kama kasa,
Akalia na kususa, eti nyie mwamtesa,
Keshalishindwa darasa, kumsomesha si ruksa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

Na pesa itamtosa, milele ikamsusa,
Abaki kula mikasa, na vingine vyenye tasa,
Rehema kutomgusa, h adi tawba kunusa,
Kila muabudu pesa, mwisho huja kuikosa!

No comments: