Saturday, March 24, 2012

Sio kila mvaa kanzu

Kanzu wengi huivaa, na sio tu waswahili,
Arabia ukiingia, vazi taifa kamili,
India waitumia, Wahindi wenye jamili,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

Wabangla wanavaa, Bangladesh ni mali,
Joto huwa lapungua, hali kuwa afadhali,
Na mimi nimenunua, kuivaa si muhali,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

Wanavaa Nigeria, Agbada wabadili,
Nakshi wamezitia, ni vazi la wenye hali,
Fukara wao huvaa, hizo zenu sarawili,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

Zipo Mauritania, wavunako petroli,
Zimejaa algeria, suti zinazikabili,
Na ukifika Libya, kuziona si ajali,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

Waganda wazitumia, kuwa nayo ni adili,
Sherehe huwa zavia, kanzu zikiwa muhali,
Na Wahaya nao pia, hili kwao bilkuli,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

Mapadrir watumia, kanisani mhimili,
Majoho rangi hutiwa, lakini hawabadili,
Kingine hawatavaa, patakuwa mushkeli,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

Mujarabu Indonesia, wenye mashati ya ukili,
PIa musuli watia, watu wenye zao hali,
Ni tabia kutojua, ukidhani udhalili,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

Waheshimu Malaysia, tajiri wenye asili,
Lugha yao imekua, na vazii lao kamili,
Husetiri yalokuwa, kuiga kwao muhali,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

China wanaitambua, ila uzungu mkali,
Ila ndani wakikaa, kingine hawabadili,
Raha yake waijua, kwani sio baradhuli,
Sio kila mvaa kanzu, atakuwa mswahili!

No comments: