Tuesday, March 27, 2012

Uoza unachosifu....

Ni makao yake nzi, uozo ukisifiwa,
Usafi kwake ajizi, na manukato kinyaa,
Kwenye zama za ushenzi, hata mtu naye huwa,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

Wanaizaya wapuzi, nzi nawalingania,
Wengine kwao viazi, na wao wanaojua,
Hawaijui miezi, na inavyopanguliwa,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

Nyakati hawamaizi, za kupwa na kujajaa,
Hawayajengi makazi, pale palipotulia,
Ila ni yao hifadhi, pale panapotitia,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

Hudhani yao hijazi, ngazi walizopandia,
Kushuka chini hawezi, wa juu kachagulia,
Na mazao na mizizi, kati yake bora huwa,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

Huyaogopa maradhi, akawa kiguu na njia,
Mauti ikawa kazi,aliko kumkimbilia,
Lakini hana ujuzi, hutua panapotakiwa,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

Hushikwa kigugumizi, Ziraili akitua,
Akawa aomba radhi, hata kwa asiyoyajua,
Ulimi ukawa ndizi, mzito kuunyanyua,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

Anachoona azizi, ndicho kinachomuua,
Na aipandayo ngazi, juu hujamuengua,
Dunia hii malazi, makazi haikujaliwa,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

Na ukimuona nzi, kwenye mvi ametua,
Ndani nywele za nyuzi, vidonda vinachipua,
Na ubongo mfinyanzi, maji yeshakuingia,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

Nihifadhi ya Azizi, njia kunichagulia,
Hakunaye kiongozi, anayekutangulia,
Na wewe ni muokozi, ingawa wakukataa,
Uoza unachosifu, ni ikulu yake nzi!

No comments: