Wednesday, March 21, 2012

Hutaka wanachotaka

Nia yao hutojua, hadi ukiwapatia,
Wapo walionuia, sahani mia kutwaa,
Wenyewe wakajilia, wakajakosa jamaa,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Wote wanaolilia, ukubwa kujipatia,
Jamii yaelekea, kingi juu inatoa,
Na chini pakabakia, kidogo kilichokuwa,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Kila mtu ang'ang'ania, na yeye juu kuwa,
Ili kwenda jipatia, huko kilichosombewa,
Huku chini waugulia, njaa inavyosambaa,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Makosa ninadhania, nchi imeshaingia,
Kingi juu kuachia, chini kidogo kikawa,
Na rivasi kuitia, naona sasa yafaa,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Kidogo kukiachia, juu huko kubakia,
Na chimi kuongezea, vijijini kwingia,
Halafu tutawajua, uchungu waliokuwa,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Hawazai, watazaa, ubunge kupigania,
Ujira mdogo ukiwa, vijiji juu kupaa,
Mwenyekiti kuambua, tatu milioni pia,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Waziri yeye kupewa, mbili milioni pwaa,
Pua kuangukia, bure juu kuelea,
Ila akivumbua, kitu watu cha kufaa,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Ila akivumbua, kitu watu cha kufaa,
Nyingi ataongezewa, kulingana manufaa,
Na mbunge naye pia, hivyo hivyo ije kuwa,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Wengi wataukataa, ubunge ninakwmbia,
Na kazi kubwa itakuwa, mawaziri kuchagua,
Vijiji watakimbilia, wilaya nayo mikoa,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

Ni mfumo waugua, na watu wana mafua,
Wote juu kukimbilia, watafuta kujifaa,
Katu ninakataa, si watu kusaidia,
Hutaka wanachotaka, kwa sababu wajuazo!

************


Ha ha ha ha haa......hili haliwezekani,
Wenye njaa wako wengi Tanzania
kuliko wanaoshiba!!!!

No comments: