Tuesday, March 27, 2012

Akujenge nani wewe

Maisha yake mafupi, mja katika dunia,
Na akili zake fupi, katika kufikiria,
Hajui katoka wapi, atang'ang'ania bua,
Akujenge nani wewe, aache jijenga yeye?

Hatari haiogopi, huogopa manufaa,
Akakamata makapi, na punje kuziachia,
Kwa udhia fotokopi, ibilisi amekua,
Akujenge nani wewe, aache jijenga yeye?

Kwa neema hanenepi, zaidi hukimbilia,
Augua yanguyapi, bidhaa hajaijua,
Na kwa ukweli haapi, shetani keshamwingia,
Akujenge nani wewe, aache jijenga yeye?

Nusura muda haipi, yake kuyapalilia,
Hali siku zake ngapi, hilo hajaling'amua,
Nahodha hamuogopi, ni yeye ajidhania,
Akujenge nani wewe, aache jijenga yeye?

Uwe ni ndugu wangapi, hali hawataijua,
Huhesabu mali ngapi, sikuhiyo zaingia,
Ukikopa hakukopi, haukopesheki baa,
Akujenge nani wewe, aache jijenga yeye?

Hawaniulizi vipi, twaweza kukusaidia,
Wangoja tangazo fupi, msibani kunijia,
Mauti huwa ni papi, nyumba zao hujengea,
Akujenge nani wewe, aache jijenga yeye?

Nimeandika kifupi, kwani nachanganyikiwa,
Nje hauvai chupi, ila ndani yavaliwa,
Na mengi kama makapi, huwezi kuongelea,
Akujenge nani wewe, aache jijenga yeye?

Ndugu zangu siwatupi, ila sintowategemea,
Yamenishinda mangapi, nao wanaangalia,
Na wengine wako 'hepi', dhiki zikinifumua,
Akujenge nani wewe, aache jijenga yeye?

No comments: