Saturday, March 24, 2012

Kila mvaa musuli

Suti wanaoabudu, huudharau musuli,
Hawawezi kuhusudu, avaacho mswahili,
Kawapitia mdudu, hali kwao sasa mali,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Shati si yangu tabia, fulana ninaivaa,
Suruwali haijawa, naona kwangu udhia,
Kwa raha ninatembea, musuli nimeivaa,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Jaani mliwatoa, mengine wahadithia,
Vazi wanalichukia, uswahili walitia,
Waona limepungua, haliwezi heshimiwa,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Hili ninalikataa, waziwazi kutetea,
Suti anayeivaa, ubora hajazidia,
Wengine tunawajua, matapeli wamejaa,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Makatili walokuwa, wengi suti wavaa,
Ovyoovyo wanaua, na kubaka ni tabia,
Hakuna asiyejua, ila zuzu walokuwak,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!



Musuli wanaovaa, ni wazuri kwa tabia,
Ndani ukiangalia, huruma wamejaliwa,
Si watu wa kugomeba, akina wapita njia,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Barizi wairidhia, ni watu wa kutulia,
Hawana hizo ghasia, za suti wanaovaa,
Baraka huzidishiwa, ibada wakiilea,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Wengine kama majuha, udini wanautia,
Mwislamu huikwambia, musuli anayevaa,
Wokovu wasiokuwa, hapa huachi wajua,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Nguo dini haijawa, na wala haitakuwa,
Ni wengi wajihadaa, na kisha kujajutia,
Wakati umepotea, kwao hubaki balaa,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Laiti ningelijua, haweshi kujisema,
Uzaini ukivaa, hatimaye utalia,
Moyo hauwezi jua, ndaniye kilichokuwa,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

Wahuni na changudoa, musuli wanaivaa?
Na wakubwa wenye njaa, waweza kuikaribia?
Polisi wanaujua, ghera hutapakaa,
Kila mvaa musuli, aachi kudharauliwa!

No comments: