Thursday, March 1, 2012

Binadamu mashetani

VITABU ukifatia, haya utayaelewa,
Mimi nahadithia, wewe utafafanua,
Isome historia, mengine yametokea:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine wake zetu!

Waweza naye kukaa, shetani hutomjua,
Sura nyingi huchukua, amka na kuamkia,
Ila unapojaliwa, waweza kumfichua:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Wengine waume zetu!

Wanasiasa mwajua, nao weza kuwa pia,
Nyie mkawadhania, malaika walokuwa,
Na kumbe kinyume wawa, nanyi hamjawajua:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Wengine wanasiasa!

Nchi ikishalaniwa, viongozi hupatiwa,
Mashetani walokuwa, na wala hamajua,
Ila yakiwaharibikia, mtabaki mnalia:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine viongozi!

Hata na wabunge pia, wanaojifikiria,
Ya wao kutoyajua, wala kuwasadia,
Bajeti wanazopewa, wajua wanavyotumia:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine ni wabunge!

Wengine huchaguliwa, hata mawaziri kuwa,
Hakuna wa kuwajua, kwa siri wajifanyia,
Ila Muumba ajua, na nchi inalegea:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine mawaziri!

Kadhalika na mikoa, kama hawa hujapewa,
Wala si wa kuchagua, juu juu hutokea,
Mkija kushtukia, mmekwishakuvamiwa:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Wapo wakuu wa mkoa!

Sura nimejisomea, na hili lahadithiwa,
Ukitaka jiokoa, kwa Mola wako rejea,
Hakuna wa kuaminia, vingine utatpotea:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Wapo wakuu wa wilaya!

Kwa baadhi ya wilaya, hawaachi kuingia,
Maliasili ikiwa, kwa sana inayong'aa,
Nao utawatambua, kwa uroho na tamaa:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Wapo wakuu wa wilaya!

Wanausalama pia, dini wasioijua,
Aghalabu kutumiwa, na wakubwa walokuwa,
Nao huja kuamua, ya kishetni nao pia:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine mapolisi!

Madaktari nao pia, wengine huondokea,
Njaa ikiwazidia, na nyenginezo taamaa,
Ushetani wakavaa, wagonjwa kuumbuliwa:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Wengine madaktari!

Mashehe hutoshangaa, nao wapo kusikia,
Njaa inapoenea, na uchu kuwachachia,
Huuza vilivyokuwa, wakfu vimeshawekewa:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine ni mashehe!

Kaumu Lutu huzua, hawa waliolaniwa,
Na vitabu wavijua, ila upofu kwingia,
Kizazi wakakifua, kisiwe chenye kufaa:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine ni mashehe!

Na wajua biblia, dhuluma huiamia,
Vya watu wakachukua, upaku wakajitia,
Wakishakugunduliwa, ni wachawi walokuwa:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine ni mishenari!

Huitembeza zinaa, huku wamezuiliwa,
Na neno walilopewa, ngono kutokuingia,
Nguvu zote huishiwa, hata watoto kukwea:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine ni mapadri!

Kulinda wanaojua, jukumu hulikimbia,
Tamaa kuwaingia, utu ukawapotea,
Wakawa washughulikia, nchi yanayoiua:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine makamanda!

Wahisani nao pia, wengi tu wanaingia,
Na wanayotufanyia, ni Mola anayejua,
Lakini wakajitia, eti ndio watufaa:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine wahisani!

Wawekezaji balaa, huja na kupwa ikawa,
Mikopo wakiichukua, na wakubwa kugaiwa,
Haraka hujitokea, miradi yao kuvia:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Wengine wawekezaji!

Weupe wamejaliwa, ila ni shetani pia,
Wazungu wakiamua, mbona mtawakimbia,
Na Wachina nao pia, huweza hivyo wakawa:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine ni Wazungu!

Mola akitangulia, hawa wote huzubaa,
Na udi ukishatia, wenyewe hujiondoa,
Uchamungu kwingia, mashetani hupungua:
Binadamu mashetani, wapo na twaishi nao:
Na wengine ni wazawa!

Machi 01, 2012
Dar es Salaam. Tanzania.

No comments: