Sunday, March 11, 2012

Hujafa hujaumbika

Zamani sikulishika, nikawa nayo hakika,
Leo lilivyojiweka, naona laeleweka,
Hakika hapana shaka, msemo wakamilika,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Sasa nina uhakika, hujafa hujaumbika,
Kiumbe huzalika, hali amekamilika,
Lakini yaja kuzuka, kiungo kikakatika,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Mapambo anayeweka, na mkorogo kunyweka,
Weupe akiutaka, avutie kina kaka,
Sumu huja kugeuka, makubwa yakamfika,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Akili aliyeshika, akawa afundishika,
Huweza akawehuka, ukichaa kumshika,
Elimu ikatoweka, awe asiyetamanika,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Utajiri huushika, Mola anayemtaka,
Mja akatajirika, na kwa sifa kusifika,
Mwisho akazuzuka, na vituko vikazuka,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Mali huja kuyeyuka, ufukara kuudaka,
Na akisha kuchachika, na kufulia hakika,
Hakuna wa kumtaka, juzi waliomtaka,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Kwa cheo hujanyanyuka, nao wakabahatika,
Kote wakaheshimika, na majina kujengeka,
Ila muda ukifika, ni lazima kung'atuka,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Cheo wanapokishika, wasioelimika,
Hufanya yao mizuka, na mengi wakaropoka,
Ila wakija kushuka, huvia kama kichaka,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Ujibari hutoweka, ikiisha mamlaka,
Kwa aliyekisifika, na akadharaulika,
Kuonekana kishoka, na asiyestahika,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

Hapahapa najiweka, kumbe sijatukuka,
Ni mja nadharaulika, kwalo ninaridhika,
Lingine sijalitaka, hapa nimekamilika,
Hujafa hujaumbika, sasa nina uhakika!

No comments: