Saturday, March 24, 2012

Taarab, taarab

Taarab Tanzania, ina kubwa historia,
Kiswahili kuzaliwa, ndipo ilipochipua,
Imetunzwa ni dia, vingine haitakuwa,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Ilyas wasikia, naye Mariamu pia,
Nyuma yenu tutakuwa, lulu haitapotea,
Na tungo kuwatungia, wasonacho kusikia,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Ally Saleh sikia, hapa ni pakushikia,
Zanzibar twaijua, lugha ilipozaliwa,
Na chogo haitakuwa, waanze kuitetea,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Nasara wameyazua, sanaa dini ikawa,
Watu wanawaambia, Waislamu watakuwa,
Nyimbo wakizisikia, nazo zikawavutia,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Uongo waliozua, hata Mola aujua,
Taarab nawaambia, ni mzizi Tanzania,
Wala dawa haijatiwa, hawawezi kuiua,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Mipasho kwetu kadhia, si raha nawaambia,
Kwa wengi hii ghasia, ijapo wavumilia,
Amri ningelipewa, mbali ningeziulia,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Matusi zimeandaa, na visasi kuvizua,
Udenda watu wajaa,ufasidi na tamaa,
Dhambi wajikusanyia, tena wakishuhudia,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Taarab maridhia, ni kijiwe chenye nia,
Mme na mke hupaa, kileleni kufikia,
Na wana ndani wakawa, ktojua wasichojua,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Maneno yanatumiwa, kupanga yaliyokuwa,
Kila unaloimbiwa, dhamira yakusudiwa,
Hakuna la kupotea, mizani yazingatiwa,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Maudhui huchukua, jamii inayojua,
Mitaani wayavaa, kila siku yatokea,
Na nyumbani yazagaa, yangoja kuchukuliwa,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Moyo huudadavua, kinywa kikazingatia,
Ulimi ukafatia, na sauti kutungiwa,
Nawe ukiyasikia, roho yanakustua,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Ni neema tuliyopewa, kuitunza twatakiwa,
Pengine kuipigania, isije kuteketea,
Yazuka yasiyokuwa, mabaya yakusudiwa,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

Ala zisije potea, dungayembe kubakia,
Twataka waliojaliwa, vipjai wakajaliwa,
Kila wakituchezea, ya kale kukumbukia,
Taarab, taarab, hakuna cha asilia!
Vingine vitu vipya,
Mipasho na rusharoho!

No comments: