Wednesday, March 21, 2012

Huwapangi wapangike

Ni jeshi la mamluki, wanaoiganga njaa,
Dhambi hawataharuki, sio wanaoijua,
Bunduki nayo mikuki, yoyote humwelekea,
Huwapangi wapangike, malengo ni tofauti!

Maisha kwao dhihaki, kuua wao tabia,
Na viungo mishikaki, sambusa nazo bajia,
Na chama chenye milki, hii ndiyo yake njia,
Huwapangi wapangike, malengo ni tofauti!

Hugawa kiunafiki, hata na wao raia,
Wapo wastahihi, nchi waishikilia,
Na wengine si riziki, kesho yao watajua!
Huwapangi wapangike, malengo ni tofauti!

Kwa wazee wanafiki, mradi kuwatumia,
Dhuluma waloshtaki, kuwadi huwazomea,
Na mkimbia kaniki, hariri hulanguliwa,
Huwapangi wapangike, malengo ni tofauti!

Wanawake wastahiki, shere huzungushiwa,
Matenge sio kaniki, neema wakaidhania,
Huku wazidi umia, na faraja yapotea,
Huwapangi wapangike, malengo ni tofauti!

Vijana huzinguliwa, matabaka kuyavaa,
Hupewa walojaliwa, na wengine kufa njaa,
Miaka ikasogea, nuru huku yapotea,
Huwapangi wapangike, malengo ni tofauti!

Kwa safu hawapangiki, si watu wa kutulia,
Njaa inavyowashtaki, lolote hulivamia,
Kama mbwa na steki, meno pingu hujatia!
Huwapangi wapangike, malengo ni tofauti!

No comments: