Saturday, March 31, 2012

Kuna harufu ya hongo

HUJIFANYA watawala, wananchi wakazuga,
Wao wakipata kula, makombo watagawa-ga,
Maua katika yala, ni sehemu ya maboga,
Kuna harufu ya hongo, kauli za viongozi!

Ila lazuka suala, lisilotaka uoga,
Kileo pia kimila, udhia tukaubwaga,
Watu wasio fadhila, nao tupate waaga,
Kuna harufu ya hongo, kauli za viongozi!

Wanaotumia hela, haki zetu kuvuruga,
Kukataa yao hila, pembeni tukawaswaga,
Wabakie wenye ala, akili wanaotumia,
Kuna harufu ya hongo, kauli za viongozi!

Zinakwama zetu hali, kwa kuyabeba maboga,
Ni wachache wa fadhili, kwayo wakishakuroga,
Hukufanza ni anzali. wakazidi kujikoga,
Kuna harufu ya hongo, kauli za viongozi!

Ya kwao sio kamili, ndio kisa wanahonga,
Na wengine majahili, hujuma wanazitunga,
Budi mustakabali, hawa tukawavuruga,
Kuna harufu ya hongo, kauli za viongozi!

Ili tupate jamali, wa kale tuwapa bega,
Tuiwashe na kandili, yaliyo bora kuiga,
Tusiwe tena mithili, viumbe wanaofugwa,
Kuna harufu ya hongo, kauli za viongozi!

Hali zetu kubadili, budi tuache kuhongwa,
Tukamhofu Adili, kiboko kutotupiga,
Tukazijenga amali, na wengine kutuiga,
Kuna harufu ya hongo, kauli za viongozi!

Tumuombeni Jalali, mabaya tukayabwaga,
Uondoke mushkeli, neema tupate oga,
Zinawiri zetu hali, utu tupate kujenga,
Kuna harufu ya hongo, kauli za viongozi!

No comments: