Wednesday, March 7, 2012

Tasihili yatakiwa, nusura kuambulia!

Ukubwa ukishapewa, kazi budi kuzijua,
Muhimu iliyokuwa, moja nitawaambia,
Ni tendo la kuamua, pasi mtu kuchelewa,
Huruma mnamwachia, tatizo kulitatua ?

Ni kazi ya kuamua, pasi mja kuchelewa,
Leo linalotakiwa, sawia kuazimiwa,
Hujua lakulijua, na yepi kuyaachia,
Imani mnamwachia, tatizo kulitatua?

Huwezi kumuachia, mwengine asiyekuwa,
Sio soka latambaa, ni uhai twaamua,
Hali chelewa, chelewa, wengi huja kuumia,
Uzalendo atajua, tatizo kulitatua ?

Na mwana hawezi kuwa, ni wako wa kumzaa,
Si riziki itakuwa, na kila mtu ajua,
Menejimenti ni nia, na nia ni kuamua,
Kiapo atatambua, tatizo kulitatua ?

Afrika tunavia, kisa chelewa, chelewa,
Leo linalotakiwa, kesho litaingojea,
Na siku zinakimbia, na wiki zazidi paa,
Ahadi anaelewa, tatizo kulitatua ?

Miezi inaishia, na miaka yaambaa,
Watu bado wangojea, kama aushi wapewa,
Na miaka twaijua, hamsini twajifia !
Midia wanalijua, tatizo kulitatua ?

Sayansi tukiijua, muda hatutachezea,
Hakuna la kungojea, miongo yayoyomea,
Pasiwe wa kuambua, maisha kinachofaa,
Sheria mnamwachia, tatizo kulitatua?

Hekima ninaitoa, kwa wakubwa walokuwa,
Dogo ukiliachia, kubwa lipate kukua,
Zimwi utajamlea, nguvu akakuzidia,
Roho nzuri atajua, tatizo kulitatua?

Machiavelli najua, busara alitumia,
Mmoja hawezi kuwa, bora kuliko ya mia,
Na hili mkilijua, wala hamtachelewa,
Uoga mnamwachia, tatizo kulitatua?

Watu wataulizia, hao sasa walokuwa,
Kitu gani wahamiwa, pengine tusichojua,
Siri gani ilokuwa, wajayo kuifichua ?
Mabavu mtamwachia, tatizo kulitatua?

Hii demokrasia, shere mnaichezea?
Ya wengi wakiamua, mnaweza kuzuia,
Hili sijalielewa, naona nachanganyikiwa,
Umoja mnamwachia, tatizo kulitatua?

Kushoto ukipitia, watapitia kulia,
Kukutana haijawa, hadi machweo yakawa,
Na hukanganyikiwa, wazidio kuumia,
Amani mnamuachia, tatizo kulitatua ?

Nafusi tukijifua, umma utateketea,
Nami ninavyotambua, Tanzania imejaa,
Mawaziri wanaofaa, hata leo kuchagua,
Mabavu mtamwachia, tatizo kulitatua?

Kupasiana ikiwa, goli bila kuingia,
Sana mtashangiliwa, mwisho mtajazomewa,
Ushindi unatakiwa, kufunga mnatakiwa,
Uchunguzi kujinoa, tatizo kulitatua ?

Rabana namwachia, ushauri nimetoa,
Watakaonisikia, yangu watayatumia,
Shukrani nitapewa, na nitakaowaokoa,
Uchama mtamwachia, tatizo kulitatua?

Tatizo kuliachia, balaa mwatutakia,
Hivi leo kuchelewa, maamuzi kuyatoa,
Twasema kiteknolojia, kwalo hilo mwafulia,
Uchama mtamwachia, tatizo kulitatua?

No comments: