Sunday, March 4, 2012

Rafiki kuwa adui

DUNIA hii hilaki, mkubwa mtafaruki,
Mambo yake ya mkiki, wala hayaaminiki,
Uendako haufiki, utokako huafiki,
Rafiki kuwa adui, na adui ni nabii!

Unaota unafiki, shamba halitambuliki,
Magugu yakahiliki, yenye kustahiki,
Pawe hapana riziki, hata kijiti cha mswaki,
Rafiki kuwa adui, na adui ni nabii!

Nafaka haziwekeki,huoza kwa taharuki,
Na ghalani hakwendeki, miiba inajinaki,
Na vyungu hatueleki, gharama hazishikiki,
Rafiki kuwa adui, na adui ni nabii!

Rafiki twamdhihaki, adui atumiliki,
Yao hayaelezeki, wajua waso fasiki,
Mja haaminiki, tena kamwe habebeki,
Rafiki kuwa adui, na adui ni nabii!

Mnfafanya dhihaki, hamjui mamluki,
Tayari keshaafiki, atoa kwao malaki,
Wasome kuja miliki, kisicho chao kwa haki,
Rafiki kuwa adui, na adui ni nabii!

Wenzi hawakereheki, baya haliwaafiki,
Meli yao haizimiki, wala haizamiki,
Fakiri ana fataki, akidhani mshikikaki,
Rafiki kuwa adui, na adui ni nabii!

Ayajua Mturuki, mtwana haaminiki,
Na kafiri ni Giriki, mikosi haiachiki,
Hugeuka mnafiki, ajiuzaye rafiki,
Rafiki kuwa adui, na adui ni nabii!

Watu hawana hamaki, mpaka wakwae kisiki,
Wakaijua hilaki, ndipo watapohamaki,
Mengi yenshafariki, tena haiwi riziki,
Rafiki kuwa adui, na adui ni nabii!

No comments: