Monday, March 26, 2012

Mzike anayekufaa

Issa ibn Mariamu, alikwishatuambia,
Unafiki kaujua, nje akawatolea,
Wote akawaambia, mfu huzikwa na jamaa,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

Haya namkubalia, siwezi kuyakata,
Ni ukweli uliokuwa, vingine haitakuwa,
Ila wasiojitambua, ukale wamekalia,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

Hofu wanaitumia, mauti yakiingia,
Usononi kuwajaa, kwa kile kisichofaa,
Hai alipokuwa, hayati walimwambaa,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

Ya mwisho ikiwadia, watu hujapigania,
Mstari mbele kua, heshima kujiondoa,
Naona kama kinyaa, na kwangu si maridhia,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

Akili watuchezea, wazima waliokuwa,
Ndio ninawaambia, hayunami asokuwa,
Ukishaninyanyapaa, ufu umeshauchukua,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

Mtu asiyekufaa, mfu kwako keshakua,
Usingoje kumchimbia, siku haitofikia,
Ruksa ukamwambaa, na yake kutoyajua,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

Viumbe tunatakiwa, kuibadili tabia,
Twendeni kiteknolojia, na chipsi kuzitumia,
Ili unayemridhia, nd'o anayekupigia,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

Makaburi kuyajua, dijito kuyawekea,
Ukibipu hurejea, ujue lilipokuwa,
Kidogo tu hujengewa, na bado mazuri yakawa,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

Wafu hai walokuwa, nao wakisharejea,
'No access' kuondoa, tena ukawaridhia,
Na wakishakubaliwa, uhai utarejea,
Mzike anayekufaa, wengine wazikwa na mfu!

No comments: