Wednesday, March 21, 2012

Nikilipika pakua

Asibaki mwenye njaa, gawia kwa usawa,
Nimeshapika pakua, na watu kuandalia,
Uchoyo sikujaliwa, malezi yalikataa,
Nikilipika pakua, asibaki mwenye njaa!

Nilikwishajitambua, mimi mrija nakua,
Si watu kuwanyonyea, ila kuwapitishia,
Na kila ninachopewa, kwenda kwao itakuwa,
Nikilipika pakua, asibaki mwenye njaa!

Siwezi kukizuia, kisiende majaliwa,
Ubahili nakataa, kwangu na pia jamaa,
Chochote kilichokua, kiwe kinajipitia,
Nikilipika pakua, asibaki mwenye njaa!

Siwezi kuikuzuia, ila kwa muda najua,
Na Razaki akijua, hili hatofurahia,
Na radhi ninaililia, vipi nije mkosea?
Nikilipika pakua, asibaki mwenye njaa!

Kazi yangu naijua, haijawa kuzuia,
Siwezi kushikilia, wengine nawaachia,
Yao wakiamua, na Mola wao wajua,
Nikilipika pakua, asibaki mwenye njaa!

Kwa ninayobarikiwa, hupewa wakatumia,
Mimi si wa kuamua, kanuni nazo sheria,
Adili nazingatia, na haki kuazimia,
Nikilipika pakua, asibaki mwenye njaa!

Vingine siwezi kuwa, haya yangu majaliwa,
Na ufakiri ukiwa, basi kwangu ni hidaya,
Na utajiri ikiwa, mzigo nazidishiwa,
Nikilipika pakua, asibaki mwenye njaa!

No comments: