Tuesday, March 27, 2012

Tabaka la watawala

Hujua wanayojua, ujinga wakaulea,
Mwana asiyejijua, mbeleko hatoachia,
Hubwebwa akanyamaa, taahira keshakua,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Mtawala hunyakua, kisicho chake kutwaa,
Kisha akagugumia, na mengine kuchukua,
Ikawa hajawaachia, akili ila udhia,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Na mchana huibiwa, jua linaangazia,
Kasumba wameshatiwa, sio wanaojijua,
Ikawa wanasifia, kikaango kilichokuwa,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Mafuta yanayotumiwa, wao kuwakaangia,
Ni yao yakamuliwa, kikaangoni kutiwa,
Na kisha huja kuliwa, kama wa bure dagaa,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Chini wanapoambiwa, kukaa wanatakiwa,
Hushindwa kuligundua, sio wa kuamriwa,
Ila wao watakiwa, amri kuja zitoa,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Wakubali kung'olewa, na wao ndio wa kung'oa,
Nafasi waiachia, wawezayo kutumia,
Usafi ukaingia, kila pembe, kila njia,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Rasilimali majuha, wadhani zimeumbiwa,
Wa juu waliokuwa, na sio wao raia,
Wakubwa wakawaachia, vipande kuvimegua,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Kura wanawaachia, wao wakasimamia,
Wakashindwa kutambua, ni wao wanaotakiwa,
Haki kuisimamia, na kuzuia kuibiwa,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Hukimbizwa kwa hatua, sungura ukadhania,
Kwa kuwa mbaya sheria, ukubwa haijaujua,
Na muda umeingia, hili kuliangalia,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Hupigwa kisha walia, kazi waliowapatia,
Wakashindwa kuelewa, kufukuza watakiwa,
Juu wao watakiwa, kila kitu kwangalia,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

Wamelala wanaliwa, wasimama wavuliwa,
Watembea wategewa, wanyanyuka, wazuiwa,
Uchumi wamekalia, wajanja wawaachia,
Tabaka la watawala, lazidi kete watwana!

No comments: