Monday, March 26, 2012

Giza zito likitanda

Kichwani limeniganda, kutokea utotoni,
Kadiri ninaipenda, naitaka maishani,
Kwalo siachi kukonda, dhoofu yangu imani,
Giza zito likitanda, lailati kadri yaja!

Giza kote linatanda, nuru hamna upenuni,
Nafsi zimejisunda, mamumunye ukubwani,
Nani wa kukupenda, kama haupo machoni,
Giza zito likitanda, lailati kadri yaja!

Nafsi imenishinda, ninaugua moyoni,
Kila nilichokilinda, hivi leo mashakani,
Sasa wanazuka nunda, waingia akilini,
Giza zito likitanda, lailati kadri yaja!

Ninajifunga mkanda, kwendelea taabuni,
Aijambo akipenda, ataniafu Manani,
Mitihani kuishinda, nikaona afueni,
Giza zito likitanda, lailati kadri yaja!

No comments: