Tuesday, March 6, 2012

Beleshi Ukipokea

Kila feli hujaliwa, masomo ndani yakawa,
Na beleshi kuchukua, maudhui yamejaa,
Nayo ni kujitambua, uhai uliyepewa,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Nayo ni kujitambua, uhai uliyepewa,
Kuwa siku hutokea, ikawa unafukiwa,
Udongo kumiminiwa, kaburini ukajaa,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Beleshi linafukua, na pia linafukia,
Uwezo limejaliwa, haliwezii kukataa,
Japo dogo lachukua, tani nyingi zilokuwa,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Huchoka anayetwaa, kazi kushughulikia,
Mengi likavumilia, kwa siri yanayokuwa,
Kadhalika likafaa, ya kheri linalopewa,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Beleshi nawe pokea, uweze kuwafukia,
Wanaokutangulia, nawe nyuma wafatia,
Imani ikikwingia, hapo umekwishakuwa,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Ukawa wafurahia, utani wajifanyia,
Na mtoto hujakuwa, hujui yanokujia,
Kuishi unadhania, hatimiliki wapewa?
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Na kila mwenye kujua, hili hulifikiria,
Je, nikishakufukiwa, nyuma nini chabakia,
Watu nilichowafanyia, wapate nikumbukia,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Wapo wanaojifaa, wao na zao jamaa,
Na wakishakufukiwa, wao nyuma hutumbua,
Cha mjinga hujaliwa, na wajanja wasokuwa,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Na waliodhulumiwa, haki wajarudishiwa,
Maajabu hutokea, Muksti mtarajiwa,
Na analoliamua, ndilo linalotokea,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Mwana tajiri huvia, ombaomba kujakuwa,
Na wa fakiri kupaa, utajiri akapewa,
Ibra zake hatua, Mughni anayoamua,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

Kila ukigeuzia, hebu tena angalia,
Kwa ulichokichukua, dhuluma tupu ikawa,
Wana ukawarudishia, urithi walioachiwa,
Beleshi ukipokea, ukumbuke kufukiwa!

No comments: