Tuesday, March 27, 2012

Watu unawakosea, ukiwafanya wajinga !

Akili kweli ni nywele, kila mtu ana zake,
Hata awe mwenye ndwele, yeye pia ana yake,
Huwezi mfanza mchele, akili usojaliwa,
Ukiwafanya wajinga, watu unawakosea!

Wengine kama mshale, na mkuki ueleke,
Yao mbele kwa mbele, kusaka chao wateke,
Hawataki misukule, na yao yaje yazikwe,
Ukiwafanya wajinga, watu unawakosea!

Si ya leo ni ya kale, na taji lao wavike,
Niliona ya Kaole, wala mbali msifike,
Mtu kuchanjwa chale, sio tu asilogeke,
Ukiwafanya wajinga, watu unawakosea!

Mtu kuchanjwa chale, sio tu asilogeke,
Wengine hufanya vile, washika wasimshike,
Na wengine mkalole, hupanga mbali wafike,
Ukiwafanya wajinga, watu unawakosea!

Ila kuishi milele, vigumu likubalike,
Sio leo toka kale, kila jambo na miko yake,
Na chunusi si upele, japo zote zikunike,
Ukiwafanya wajinga, watu unawakosea!

Si mtu wa makelele, ya kwangu yaimbike,
Napenda vigelegele, ila si vyenye makeke,
Inanibana tungule, kwenye chakula usiweke,
Ukiwafanya wajinga, watu unawakosea!

No comments: