Monday, March 26, 2012

Nchi inao wenyewe

Nasi tumewasikia, kwa siri wayasemayo,
Nchi waishikilia, hakunao wengineo,
Hawawezi iachia, mbwa watawale wao,
Nchi inao wenyewe, sisi tukae pembeni:
Ndivyo wasemavyo wao!

Haraka waliamua, lao kuwa ni chaguo,
Macho walipofungua, walopewa ufunuo,
Ukweli wameujua, kwa Mola ni marejeo,
Nchi inao wenyewe, sisi tukae pembeni:
Ndivyo wasemavyo wao!

Dhambi ukiitumia, matunda yake ni hayo,
Uoza ukiingia, samaki wote si zao,
Na uongo ukishakua, baraka si tena yao,
Nchi inao wenyewe, sisi tukae pembeni:
Ndivyo wasemavyo wao!

Ujanja watatumia, ila ovyo mwendo wao,
Hakuna lakuchanua, hunywea maua yao,
Rangi waweza jipakaa, chakavu majengo yao,
Nchi inao wenyewe, sisi tukae pembeni:
Ndivyo wasemavyo wao!

Afu keshawakimbia, kwa hivyo vituko vyao,
Na wakiziomba dua, madogo mapato yao,
Jalia huwajalia, ukweli wauuchao,
Nchi inao wenyewe, sisi tukae pembeni:
Ndivyo wasemavyo wao!

Walizojilundikia, huliwa na mchwa wao,
Mikosi nayo balaa, ikaribu na wao,
Marashi wakijipakaa, bado uvundo wanao,
Nchi inao wenyewe, sisi tukae pembeni:
Ndivyo wasemavyo wao!

Dhuluma yawaumbua, kwa kuwatenga wenzao,
Vyote wanagugumia, hakuna libakiayo,
Usoro wapalilia, heshima si tena yao,
Nchi inao wenyewe, sisi tukae pembeni:
Ndivyo wasemavyo wao!

Ndiye unayechagua, viongozi wetu hao,
Dhambi tumekufanyia, ni zawadi tupewayo,
Ghali sana imekua, sasa budi marejeo,
Nchi inao wenyewe, sisi tukae pembeni:
Ndivyo wasemavyo wao!

No comments: