Saturday, March 31, 2012

Mtaji ni kama mbegu

Ukifa hautokuwa, mtaji inavyokua,
Kitu hakitobakia, kufilisika ni njia,
Na ukishakuishiwa, mengi yatakusumbua,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

Talanta ukijaliwa, budi kuziangalia,
Tofauti ukajua, na hela iliyokuwa,
Kuguswa kutoridhia, salama mkabakia,
Jina mchoyo ukipewa, kubali na kuridhia,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

Mtaji mizizi hutoa, ndipo panapoanzia,
Hapo ukishikilia, chini hutotumbukia,
Ila ukja legea, pabaya utaingia,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

Mtaji wataka kulea, na maji kuumwagia,
Na hesabu kuzijua, unavyotakiwa kukua,
Usije ukapungua, nakisi ukaingia,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

Mtaji wataka mbolea, na samadi kuitia,
Na udongo kubambua, k isha ukadadavua,
Na dawa kuumwagiwa, wadudu kutokaribia,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

Kitu ukishagundua, mwenyewe kujifanyia,
Ndugu kutowaachia, na rafiki na jamaa,
Wengi waharibikiwa, watu kutumainia,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

Mtaji umeumbua, tajiri walodhania,
Wakajikuta nazaa, imekwishawachezea,
Hakuna wa kulmlilia, yazidi sepa dunia,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

Kila wakifikiria, uzembe wawashtakia,
Laiti wangelijua, mtaji wasingetoa,
Mchomgoma umekua,kushuka ukikataa,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

Kidogo ukidokoa, huwezi kurudishia,
Huwa kama ni balaa, ukianza nyong'onyea,
Dhiki hukukimbilia, wengine kuwakimbia,
Mtaji ni kama mbegu, ukiula haukui!

No comments: