Saturday, March 24, 2012

Uhuru hakika bado

Nani amekuhadaa, eti huru umekuwa,
Mimi hilo nakataa, utumwa najionea,
Lingine sintosikia, hadi nikijikomboa,
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

Bendera inapepea, wengine wajipepea,
Riziki walojaliwa, wao wanashangilia,
Njaa iliyotujaa, nini cha kujivunia?
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

Na WAONGO wamekuwa, ovyo wanajisemea,
Eti ajira zajaa, mpya wametuletea,
Ni kipofu nimekua, bado sijazigundua?
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

Zamani tukizania, nchi itatuokoa,
Ndio kwanza imekua, sasa inatufukia,
Madini wakichimbua, ni sisi tunaingia,
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

Shari imeshakua, kila pembe Tanzania,
Watu wanagugumia, kilio kinakataa,
Na sasa tunaugua, gonjwa la kuchimbuliwa,
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

Haiwi na haitkuwa, uhru kujipatia,
Bila uchumi kutwaa, mitaji kupalilia,
Mali tukashikilia, za kweu tulizojaliwa,
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

Ardhi tukianzia, yafaa kutukomboa,
Bei nzuri twaijua, siyo hii tunayopewa,
Ya sasa watuibia, na wao wote wanajua,
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

Migodi wangenunua, halali wakalipia,
Fedha yao kutimia, matajiri tungekuwa,
Ila tunaongopewa,vibaya tunalalaliwa,
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

Tumuombeni Jalia, nusura kutupatia,
Na haki akaridhia, na sote kutufikia,
Na mwaka ukiingia, aweze kutunyanyua,
Uhuru hakika bado, hadi uchumi kutwaa!

No comments: