Tuesday, March 27, 2012

Haki kwavyo ving'amuzi

Wakubwa naulizia, vigezo walivyotumia,
Haki ya kutuuzia, ving'amuzi Tanzania,
Umma mmechukua, na walokole walokuwa?
Haki kwavyo ving'amuzi, mbona hamuwapi wengi?

Madhehebu naulizia, zingine zilizokuwa,
Mbona hamkuchagua, au kweli wameishiwa,
RC na Islamiya, wameshindwa kulipia?
Haki kwavyo ving'amuzi, mbona hamuwapi wengi?

Nao kina Ahmmadiya, na ina Ismailia?
Nako mashambani pia, vipi mtakufikia?
Za simu natarajia, kampuni zingefaa,
Haki kwavyo ving'amuzi, mbona hamuwapi wengi?

Mitaji tukipatia, vijana wa Tanzania,
Tivii kujiundia, hivi hawataridhia?
Twendelee kununua, mapinduzi yeshaingia?
Haki kwavyo ving'amuzi, mbona hamuwapi wengi?

Ajira twazililia, nyie mnaziachia?
Ipo teknolojia, Tivii kujiundia,
Mbona mnachelewa, au mmekusuidia?
Haki kwavyo ving'amuzi, mbona hamuwapi wengi?

Masafa kutuchia, mikoa huru ikawa,
Hilo mmeshaamua, au amri mwangojea?
Karne imeshaingia, Tivii kukosa karaha,
Haki kwavyo ving'amuzi, mbona hamuwapi wengi?

Na uhuru mwatakiwa, watu mkatuachia,
Nyie ni kusimamia, na si kutuingilia,
Ushauri nautoa, mwapaswa kufikiria,
Haki kwavyo ving'amuzi, mbona hamuwapi wengi?

No comments: