Sunday, March 11, 2012

Hujawa mtoa riziki

Kumbe ungelipewa, kazi riziki kutoa,
Watu wangeliumia, na viumbe kujifia,
Uchoyo kukuingia, na kisasi kulipizia,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

Wewe kiumbe tambua, riziki hutoitoa,
Kiasi umegawiwa, kwa muda kuanglaia,
Ni mrija ulokuwa, riziki inapitia,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

Jaziba ikikujaa, Razaki kujidhania,
Watu ukawafanyia, yasiyokustahilia,
Ujue unapotea, mja utaangamia,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

Haukuwa na ukawa, umekua, hutokuwa,
Muda unajipitia, nao utakuondoa,
Hakuna anayekaa, milele kwenye dunia,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

Hili ukilitambua, lazima uje kunywea,
Ukweli kuugundua, thamani hutonizidia,
Hata ukinizidia, hapahapa yaishia,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

Jalali namuangalia, na yake ninahofia,
Hakuna wa kunizuzua, pengine nikahamia,
Namridhi nikijua, na yeye ataniridhia,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

Sharifu namsifia, Modhari aliyekuwa,
Aliponiangalia, na tasbihi kupewa,
Na dini nikaijua, na mapenzi kunijaa,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

Kwa Mola namuombea, peponi kutangulia,
Ghorofa akalipewa, dhahabu lililojengewa,
Na yote kuridhiwa, kiumbe aliyetimia,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

Nasi tuliobakia, wenyewe twajiombea,
Hata kitone kufaa, jana kwenda kuingia,
Mola akaturidhia, iwapo twamridhia,
Hujawa mtoa riziki, na wala hautokuwa!

No comments: