DINI wasioijua, huwatakiwa mabaya,
Rafiki waliokuwa, na ndugu pia mabaya,
Bila ya kujang'amua, huweza kuwarudia,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Tabia hii ambaa, nuksi kwako itakuwa,
Kila unayemtakia, mwenyewe hukurudia,
Ukawa usiyejua, kwa yanayokutokea,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Usiwaombee mabaya, wakutendao ubaya,
Kawaombee radhia, mema yanayoakiwa,
Waache wao ubaya, na Mola wakamjua,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Hizi njema kubwa dua, lakini zatahiniwa,
Wakutendao ubaya, jema weza kuwa baya,
Na kila ikibadiliwa, huwa ndiye yeye mbaya,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Wasaa wako tumia, bwana wako kumjua,
Soma na kushuhudia, fahamu na kutambua,
Tawhidi zingatia, na usije iachia,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Waache wako wabaya, mabaya wakayavua,
Leo wanafurahia, kesho watayalilia,
Leo wajilimbikizia, kesho yatawatumbua,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Wale wanaotumiwa, wema wakawaumbua,
Hao marudufu huwa, adhabu kwenye dunia,
Na huja kuumbuliwa, na watoto waliokuwa,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Hicho wanachokipewa, huja sumu kugeukia,
Wana wanapozaliwa, tayari wenshapewa,
Wajukuu wao pia, wabaya kabisa huwa,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Ukubwani hulemaa, na kisirani kikawa,
Wasiwe wa kuvumiliwa, waonekane kinyaa,
Hata na waliowazaa, tumboni wakawatoa,
Takiya mtu mabaya, mwisho hukupata wewe!
Saturday, March 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment