Saturday, March 10, 2012

Ni kinyozi wa vinyozi

CHAMA mbwani sasa sumu, waidhulumu kaumu,
Mengi wanakituhumu, yalojaa udhalimu,
Kila pembe na sehemu, inatoka milizamu,
Chama kikitaka moja, wape, beba milioni!


Asubuhi hujihimu, vya umma kuvidhulumu,
Kwa kujipa umuhimu, na mengine ya haramu,
Wenyewe kujikirimu, vya wengine visidumu,
Chama kikitaka moja, wape, beba milioni!

Ukubwa unagharimu, wahasibu watuhumu,
Memo zinazosalimu, kwa wizi zatakadamu,
Ni vijinga vya haramu, moto vinajihukumu,
Chama kikitaka moja, wape, beba milioni!

Sicho tulichokifahamu, kwa yake kubwa nidhamu,
Mamluki wajihimu, na nchi kuihujumu,
Haisalimiki kaumu, kujua hili adhimu,
Chama kikidai kumi, wape, kata bilioni!

Maisha yatugharimu, badala ya kukirimu,
Wachache wameshaazimu, kutunyonya yetu damu,
Yapasa kwenda kiamu, kadiri kuihujumu,
Chama kikiomba mia, wape, vuna trilioni!

Salama haitusalimu, natabiri madhulumu,
Ijapo si mnajimu, hii niwazi beramu,
Yatangaza binadamu, kwetu sasa si muhimu,
Chama kikitaka moja, wape, beba milioni!

Wanasiasa wakimu, sala zenye udhalimu,
Waiburuza kaumu, umbumbumbu ukidumu,
Kwa wasiyoyafahamu, wao waliyoazimu,
Chama kikidai kumi, wape, kata bilioni!

Wataka kujikirimu, kwa jasho na pia damu,
Kasma yao ghulamu, kutegeuza hadimu,
Kwishi kama marehemu, badala tusiwe hamu,
Chama kikiomba mia, wape, vuna trilioni!

Silioni ni adimu, katika mastakimu,
Nafata mustaqimu, na kadiri ya adhimu,
Maamuma kujihimu, hili watatakadamu,
Chama kikitaka moja, wape, beba milioni!

Ni kinyozi baragumu, napuliza kwa hasimu,
Wakifanzia kaumu, wengine wawadhulumu,
Wajigeuze hadimu, wakidhani mahakimu,
Chama kikidai kumi, wape, kata bilioni!

Yaafiki ya Karimu, uchama kuuhujumu,
Usiathiri kaumu, kwa uroho na haramu,
Nchi ipate kudumu, si vyeo na udhalimu,
Chama kikiomba mia, wape, vuna trilioni!

No comments: