Saturday, March 24, 2012

Kachague mgombea

ARUMERU nawambia, yaingia KOMKYA,
Usingizi nawatoa, mkweli mnayenijua,
Ni huru niliyekuwa, hakuna cha kutumiwa,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

Kachague kuendelea, na sio kuja tumiwa,
Yenu mtayapalilia, wazawa mliokuwa,
Kufumba na kufumbua, mtaokoa wilaya,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

Mwapasa jitegemea, sio kuwategemea,
Dhamana waliyopewa, deni kwenu halijawa,
Ujanja wanatumia, kitanzi watawatia,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

Serikali haijawa, tajiri kwenye dunia,
Nayo inachangiwa, kodi inazochukua,
Na nyingine zapotea, ubadhirifu ukiwa,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

Kidogo mkichangia, mwaweza kujinyanyua,
Na misaada kufatia, wema wanapotokea,
Njia hamtapotea, mtazidi endelea,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

Uhuru mnatakiwa, wa kiuchumi kupewa,
Nanyi sana mwasifiwa, nchi yawatambua,
Mashujaa mlokua, mkoloni kumvaa,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

Wameru ni mashujaa, haki zao wanajua,
Mababu zenu radhia, mtu hawakumtegemea,
Wenyewe walijitoa, kimasomaso ikawa,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

Ardhi kuikomboa, kina Mbise nawajua,
Na ndugu wakapokea, hazina iliyokuwa,
Aluta kuendelea, hadi leo Tanzania,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

Ni uongozi twajua, hatua ulochukua,
Chama hakikutokea, miye ninachokijua,
Ni hao wenu shujaa, mwatakiwa kufukua,
Kachague mgombea, sio CHAMA kuchagua!

No comments: