Monday, March 26, 2012

Taifa lenye uongo

KABLA hatujasogea, jambo nimeazimia,
Kongamano latakiwa, ukweli kuzungumzia,
Adili tukaanzia, na mengine kufuatia,
Taifa lenye uongo, halimpendezi Mola!

Wakubwa wazungumzia, kama yangu kurudia,
Waongo tumeshakuwa, Taifa linahujumiwa,
Juu ulishaanzia, na chini unafikia,
Taifa lenye uongo, humchukiza Mola!

Mkuu aandikiwa, uongo ajisomea,
Kisha aukubalia, taifa kutangazia,
Wacheka hata majuha, nazaa kuuparamia,
Taifa lenye uongo, halimpendezi Mola!

Wabunge waongopewa, ridhaa wanaitoa,
Labda posho watetea, isije kupungua,
Ndivyo tulivyokua, na hapo tumefikia,
Taifa lenye uongo, humchukiza Mola!

Waziri akishajua, uongo wakubaliwa,
Na chama kilichokuwa, na makada wake pia,
Na yeye atajizoa, ukumbini kuingia,
Taifa lenye uongo, halimpendezi Mola!

Na yeye atajizoa, ukumbini kuingia,
Hoja zilizotafitiwa, akazipinga kwa riha,
Naona ni ukichaa, hapa tulipofikia,
Taifa lenye uongo, humchukiza Mola!

Heshima imepungua, mzee ninawaambia,
Kioja mmeshakua, wapi mguu mtatia?
Matope mwajipakaa, mwadhani poda imekua?
Taifa lenye uongo, halimpendezi Mola!

Ni haya kufuatia, kongamano nanuia,
Adili waliojaa, mkono naungojea,
Hatua kuzichukua, likafana kila njia,
Taifa lenye uongo, halimpendezi Mola!

Huko tutazungumzia, maadili Tanzania,
Kwa ukweli kuanzia, serikalini ukawa,
Iwe kuvunja sheria, uongo wakiutoa,
Taifa lenye uongo, humchukiza Mola!

No comments: