Saturday, March 24, 2012

Udugu macho na mikono

Mkono ukiumia, macho lazima kulia,
Uchungu huusikia, kama ndiye kaumia,
Akampooza radhia, milizamu kumwachia,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Mkono hunyanyuliwa, na mwenzi aliyekuwa,
Hadi juu kufikia, macho akamhurumia,
Machozi huyaondoa, kwa kumfuta sawia,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Usilie umwambia, vizuri naendelea,
Mola ukiniombea, kazini nitarejea,
Macho akiyasikia, furaha hujamwingia,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Wengine huulizia, hali inavyoendelea,
Wapate kuwasaidia, wenzi waliozidiwa,
Msaada huutoa, hata pia kwa wabaya,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Kisha watayashukia, ya kwao kujifanyia,
Kila mmoja akiwa, moyo wake maridhia,
Ndivyo walivyojaliwa, rafiki wanavyokua,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Adimu mtu ukawa, na rafiki wa kufaa,
Wengi ni wa manufaa, na nafsi zenye njaa,
Ukishawasaidia, nawe mbali hupotea,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Hakuna wa kurejea, hali akakujulia,
Ya kwao huzingatia, ya kwako yakaishia,
Wengine hukukimbia, kila ukiwatokea,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Haya nimekwishajua, na sasa nimezoea,
Wahenga nawakubalia, tenda wema, sepa raha,
Njia ukishawaachia, mwisho nao hufikia,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Moyo hautoumia, yapo usipozingatia,
Wazuri waliokuwa, na wabaya nao pia,
Kiumbe ukitambua, mtu si wa kutegemea,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Kiumbe ukitambua, mtu si wa kutegemea,
Yake ameshaandikiwa, na kalamu hufatia,
Vinginevyo itakuwa, ya kwako yake yakawa,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Tamati nimefikia, mbele sintoendelea,
Ujumbe nimeutoa, nadhani umewafikia,
Mimi kiguu na njia, wema kwenda kuutoa,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

Namshukuru Jalia, kwani aniangalia,
Malipo yake radhia, ndiyo ninayongojea,
Watu nimewazoea, na hisani naijua,
Huu hakika wa kweli, udugu macho na mikono.

No comments: