Saturday, March 31, 2012

Unavuta blanketi

Kiasi ungelijua, yako ungeliyapima,
Yasipate kupungua, au kuzidi kasima,
Katikati ukatua, ungali bado wahema,
Unavuta blanketi, jua lakuamkua?

Muda unapoachia, yaweza zuka nakama,
Hili ukatangulia, na yale yakasimama,
Subira wasiokuwa, ndipo hapo hulalama,
Unavuta blanketi, jua lakuamkua?

Usingizi kuugua, ukizidi unauma,
Hali ikawa ni mbaya, pasiwe tena uzima,
Na haSa pakuzingatia, palipo na ndarahima,
Unavuta blanketi, jua lakuamkua?

Muda wataka tambua, umuhimu kuupema,
Na kila linalokuwa, nafasi ukaisoma,
Na somo ukalitoa, bila kuvunja kalmima,
Unavuta blanketi, jua lakuamkua?

Na usipojitambua, hili kwako si lazima,
Ila yatakayotokea, ujumbe zitautuma,
Na haki ukaridhia, bila vingine kusema,
Unavuta blanketi, jua lakuamkua?

Huwezi ukaelwa, muda wake mahakama,
Haukufuli rufaa, na masmaha kuchuma,
Hutoka ukaishia, hakuna kurudi nyuma,
Unavuta blanketi, jua lakuamkua?

Muumba wa zetu sanaa, namshukuru Adhama,
Nami nililopangiwa, kwa wakati kutazama,
Chumo nikajichumia, pahala pema kusimama,
Unavuta blanketi, jua lakuamkua?

No comments: