Tuesday, March 6, 2012

Kuona na kusikia

VIUMBE tumejaliwa, akili kuzawadiwa,
Hapa kinachobakia, namna ya kuzitumia,
Na wanaobarikiwa, katiti kuongezea,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Kati wanaoishia, akili ni kuambiwa,
Uongo wakachukua, na uamuzi kutoa,
Bila ya kuulizia, yule anayesingiziwa,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Manani humchafua, haya hatofurahia,
Adili katuambia, muhimu kuitumia,
Tusiwe wa kutulia, haki tusipotumia,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Kusoma wasiojua, wapo tele wamejaa,
Ila kwa kuangalia, elimu wajipatia,
Na wengine husikia, watu na redio pia,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Na wengine husikia, watu na redio pia,
Digrii wakachukua, ya hii yetu dunia,
Makubwa kujifanyia, kuwashinda maprofesaa,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Elimu tunayopewa, kitu haitasaidia,
Kama ispoingia, na akilini kukaa,
Tukawa tunachambua, vipi tunaitumia,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Elimu huwa walewa, wengine waliopewa,
Mvuke kuwageukia, isiwe kitu kufaa,
Wakawa wajikokea, moto unaokolea,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Lazima kujionea, akilini kuingia,
Hasa msiyoyajua, au kuyaaminia,
Maarifa kununua, kwa bei isiyokuwa,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Tivii mkiangalia, mengine yatawafaa,
Yake mkiyasikia, mtaipiga hatua,
Baada ya kutumia, lazima kuendelea,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Wakawa wajikokea, moto unaokolea,
Kiama kikiingia, huko wende kutupiwa,
Hasara kwao ikawa, mipaka isiyokuwa,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

Ninakuomba Jalia, utakayo kuyajua,
Na akilini kukaa, nipate kuyatumia,
Na siku ya manufaa, nami niwe ni shujaa,
Kuona na kusikia, ni njia za kujifunza!

No comments: